Jumapili, 20 Septemba 2015

JE WAKRISTO WANAFAHAMU MAANA YA BIBLIA ?

Somo la leo:
By : Mtumishi BAB G POWER 

JE WAKRISTO WANAFAHAMU MAANA YA BIBLIA?

TAFSIRI YA NENO BIBLIA : -
- Biblia ni maandiko matakatifu ya Mungu.

- Biblia imegawanyika katika sehemu kuu mbili
 A). Agano la Kale
 B). Agano Jipya

Ufafanuzi kwa ufupi kuhusu ( A ) Agano la Kale :-
- Agano la Kale ni kitabu kilicho wakilishwa na Mtumishi wa Mungu Musa kwa maana zaidi Musa ndiye muasisi mkuu wa Agano la Kale.

Ufafanuzi kwa ufupi kuhusu ( B ) Agano Jipya.
- Yesu Kristo ndiye mwakilishi wa Agano Jipya kwa maana zaidi Yesu Kristo ni muasisi wa Agano Jipya. 

- Biblia yote kwa ujumla ina vitabu 66.

- Agano la Kale ambalo muasisi wake ni Musa lina vitabu 39.

- Agano Jipya lenye vitabu 27 muasisi wake ni Yesu Kristo.

- Biblia yote kwa ujumla imeandikwa kwa msaada mkuu wa mafunuo ya Roho Mtakatifu.

- Roho aliyetenda kazi na Musa nyakati za Agano la Kale, ndiye aliyetenda kazi na Yesu Kristo nyakati za Agano Jipya, vile vile ndiye Roho huyo huyo aliye tenda kazi na Mungu wakati wa kuumbwa ulimwengu, pia ndiye Roho huyo huyo anaye ishi ndani ya Wakristo wanaomwamini Yesu Kristo katika Kizazi hiki.

- Kuanzia nyakati zote zilizo tajwa kwenye pointi ya juu, hakuna wakati ambao huyu Roho alionekana waziwazi na katika nyakati zote alijidhihirisha kwa wahusika katika mazingira ya kiimani kupitia Neno la Mungu (Biblia).

- Mkristo mwamini anapo iamini Biblia maana yake ameingia katika Agano na Roho Mtakatifu, kwa lugha nyingine amekubali kuongozwa na sheria ya Roho Mtakatifu.

- Nikiwa ni mtu ninaye amini maneno ya Mungu(Biblia) lazima nitambue kila Neno lililopo kwenye Biblia liko hai, yaani Lina uwezo wa kuyabadilisha maisha yangu muda wowote na kuleta uzima wa milele. (2Timotheo 3:1-17).

- Neno linashindwa kufanya kazi kwenye maisha ya mtu kutokana na udhaifu wa Imani alionao mtu katika kuamini maneno ya Mungu, ndio maana wakristo wengi humsema Roho kwa maneno lakini hawana ujasiri wa kumtumia Roho awazalishie faida.

- (Hili ni ANGALIZO nikiwa mkristo mwenye nia mbili ni vigumu kufaulu maisha. (Yakobo 1:6b).

- Baraka inayotokana na Neno la Mungu ni baraka ya milele.  ( Warumi 14: 23 )

- ( Hakuna mahali popote kwenye Biblia kunakoonyesha Roho Mtakatifu alishindwa, bali tunaona Roho Mtakatifu ndiye aliyekuwa msaada kwa mitume wote na manabii ).

- Inatakiwa niwe na Imani sana katika Neno la Mungu kwa sababu ninaye mtegemea ana umbo la kiroho na anafanya kazi katika mazingira ya kiroho.

- Tafuta upako wa Neno popote utakapo kanyaga utanyenyekewa.

- Neno la Mungu ni Agano la Mungu na mwanadamu kupitia Roho Mtakatifu, ndio maana likaitwa Agano la Kale na Agano Jipya.

Katika Biblia kuna Misingi mikuu 3,

- Hii misingi 3 iliyoko ndani ya Biblia ndiyo inayonifanya mimi kuwa hai kwa Mungu, vile vile kuwa wa thamani machoni pa Mungu.

- Msingi wa 1 ulioko ndani ya Biblia ni Upendo.

- Msingi wa 2 ulioko ndani ya Biblia ni Imani

- Msingi wa 3 ulioko ndani ya Biblia ni Utoaji, 
Haya ndio mambo makuu matatu yaliyo ibeba Biblia Takatifu, na mkristo atakaye weza kusimama sawa sawa katika misingi mikuu mitatu, njia ya kuurithi ufalme wa Mungu ipo wazi.

Ufafanuzi kuhusiana na msingi wa 1 UPENDO

NGUVU YA UPENDO:

- Ninafahamu mengi kuhusu Upendo na nimejifunza mengi kuhusu Upendo, lakini wakristo tulio wengi hatujafahamu nguvu ya Upendo.

- Upendo wa kweli na usiokuwa na doa ndani yake unatokana na mahusiano mazuri aliyo nayo mwamini na Roho Mtakatifu kupitia Neno la Mungu, kwa maana zaidi Upendo wa kweli Unatoka kwa Roho Mtakatifu ndio maana inatakiwa niweke Agano kati yangu mimi na Neno la Mungu ili uwe mwanzo wa Upendo hai kuzaliwa katika maisha yangu.

- Upendo wa kweli katika maisha ya mtu unazaliwa na Neno la Mungu, hii yote inatokana Neno ni kweli na Haki.

- Upendo wa kweli hauna nyakati maalumu nyakati zote umesimama kikamilifu yaani wakati wa shida umesimama na wakati wa raha umesimama na huyo ndio Mungu.

- Upendo ni Roho kamili ya Mungu, ndio maana Biblia imeupa Upendo kipaumbele katika maandiko matakatifu (1 Wakorinto 13:13 ) soma yote.

- Kuna Sifa nyingi za Upendo wa kweli na ambao chanzo chake ni  Mungu kuanzia mstari wa 1 mpaka mstari wa 7 wa 1Wakorinto 13, hizo zote ni maelezo ya Sifa za Upendo.

- Dunia tunayo ishi sasa hivi ili tuweze kukabiliana na vita vya kiroho tunahitaji kina cha Upendo wa KiMungu ndani mwetu, kwa sababu jamii kubwa iliyo tuzunguka sio ya waamini.

- Mambo ya Mungu hayaitaji  maigizo, bali mambo ya Mungu yanahitaji uhalisia.

- Katika maisha yangu kama mwamini inatakiwa Upendo niupe kipaumbele kwa sababu Roho Mtakatifu anaishi kwenye moyo wa mtu mwenye Upendo.

- Mkristo mwenye Upendo hai huwa na mambo 2 ndani mwake;
 A). Hekima 
 B). Busara

- Mkristo aliye kamilika katika maneno ya Mungu vile vile amekamilika katika Upendo halisi wa Mungu, kwa hiyo Roho ya shetani haiwezi kupata mpenyo katika maisha yake hata siku moja  Biblia inadhibitisha maneno haya.  (1 Yohana 4:17-18 ). 

- Kitu cha kuchunga katika maisha ili nibaki katika nguvu ya Upendo ni hofu, kwa sababu hofu ina tabia ya kubadilisha mwelekeo wa maono ya mtu, yaani mahali ambapo mtu anatakiwa kufanikiwa akiingiza hofu amebadilisha mwelekeo wa Maono hayo. 

NINI KIFANYIKE NIDUMU KATIKA UPENDO ?

- Ili niweze kudumu katika Upendo inatakiwa nisome Biblia kwa umakini ili niweze kufahamu kwa undani tabia za Yesu Kristo kwa sababu katika Biblia Yesu Kristo ni Nabii ambaye hakuonekana na dhambi wala udhalimu kutoka katika kinywa chake kwa hiyo nikijifunza kwake itakuwa ni rahisi kudumu katika Upendo halisi wa KiMungu.

- Maisha ya ukweli ndiyo yanayo tunza Upendo wa Mungu ndani ya mtu.

- Yesu Kristo aliishi maisha ya ukweli ndio maana Upendo wake ulikuwa halisi kwa watu wote.

Kuna njia ambazo naweza nikazitumia kuulinda Upendo usinajisike ndani mwangu :-
 1).Kujifunza kumsikia Roho Mtakatifu
 2).Kutii sauti ya Roho Mtakatifu.
 3).Kusimamia mwongozo ninao pewa kwa ajili ya maisha yangu

Ufafanuzi kuhusiana na msingi wa 2 IMANI.

NGUVU YA IMANI:-

- Nimejifunza mengi kuhusu Imani, na inafahamika wazi Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo ni bayana ya mambo yasiyo onekana vile vile ni kitu halisi cha Rohoni.

- Imani ni hali fulani inayo patikana kwenye Neno la Mungu katika mazingira ya Rohoni, ndio maana Imani inatenda kazi katika mazingira ya kiroho.

- Jambo lolote ninalo liamini ndani mwangu nikalikusudia lazima litadhibitika, kwa sababu Imani inafanya kazi katika mazingira magumu yaani mazingira yaliyo shindikana.

- Mkristo inatakiwa roho yake ielimishwe na Neno la Mungu ili Imani yake ipevuke kwa mambo ya kiroho kwa sababu Imani inamtaka mtu jasiri.

- Neno la Mungu linatenda kazi na Imani ya Mkristo anaye liishi, hata Mungu alionya kupitia kinywa cha Paulo mtume kwa ( Waebrania 11:6 ). 

- ( Nikiona nimekosa mtiririko wa maombi hiyo ni picha wazi kwenye ulimwengu wa Roho mamlaka yangu imekwisha pigwa na shetani, kwa hiyo inatakiwa nimtafute Mtumishi wa Mungu mwenye kina cha maombi anifungue ) 

- ( Kazi ya hisia ni kuharibu makali ya Imani ya Mkristo ndio maana Kanisa la leo limetoka katika Roho limerudi katika hisia )

- Ni vigumu kufanikiwa kupita kiwango cha Imani niliyo nayo, kwa hiyo Nikitaka mafanikio zaidi inatakiwa niongeze Imani yangu.

- Imani ni daraja la kumvusha mtu kumpeleka katika anga za mafanikio.

- Mafanikio yapo katika mazingira ya aina 2 
 A). Mafanikio ya kiroho 
 B). Mafanikio ya kimwili.

Ufafanuzi kuhusiana na msingi wa 3 UTOAJI:-

NGUVU YA SADAKA:-

- Umasikini uliokithiri katika maisha ya wakristo ni kwa sababu hawajui namna ya utoaji wa sadaka katika madhabahu ya Mungu.

- Sadaka ni Agano kati ya mtu na madhabahu ya Mungu.

- Sadaka inanguvu ya ushawishi kwenye uso wa Mungu, cha ajabu wakristo walio wengi hawatambui uthamani wa sadaka, ndio maana hawaonagi umuhimu wa kutoa sadaka katika nyumba ya Mungu

- Sadaka ni ukamilifu wa ibada katika madhabahu ya Mungu, na katika kitu ambacho kingelitakiwa wakristo wakifanye kwa nguvu zao zote ni katika utoaji wa sadaka kwa sababu uchumi wa Kanisa unategemea sadaka?

- Wakristo wengi kwenye nyumba ya Mungu wanapata baraka zao kutokana na utoaji wanao ufanya ndani ya madhabahu ya Mungu, kwa sababu hakuna njia nyingine ya kubarikiwa  nje na sadaka.

- Sadaka ni kipimo kinacho onyesha wazi ufahamu alionao mkristo katika kumjua Mungu hili jambo lilimkuta Mtumishi wa Mungu Ibrahimu.

- Chochote ninacho kitoa iwe ni kwa Mungu, iwe ni kwa mtu jina lake ni sadaka, kwa hiyo nikitambua nguvu ya baraka iko ndani ya sadaka inatakiwa niongeze kiwango changu cha utoaji sambamba na alivyosema kwenye kitabu cha  ( 2Wakorinto 9:6-7 )

- Jambo la kufahamu huwezi kubarikiwa kupita kiwango cha unavyo toa .

- Jicho la Mungu linaingia wivu na mtu ambaye ametoa sehemu ya mali yake kusapoti kazi ya Mungu hata Biblia imelizungumza jambo hili. ( Mithali 3:9-10 ).

- Baraka ya uchumi inatokana na jinsi mtu anavyo jiunganisha na madhabahu kwa njia ya sadaka.

- Nikitengeneza mikakati ya kuweka sehemu ya Mungu katika kila kipato ninacho Kipata hiyo mikondo ya baraka haita zuilika na kitu chochote.


- Wakristo wengi wanapenda vitu vya uongo kwa sababu ni wavivu wa kuutafuta ufahamu kupitia Neno la Mungu. 

Hakuna maoni: