Jumapili, 26 Aprili 2015

AMINI KATIKA NENO LA MUNGU SEHEMU YA PILI


AMINI KATIKA NENO LA MUNGU
SEHEMU YA PILI
Neno la Mungu inatakiwa lianze kujengewa mizizi ndani ya familia yangu ikiwa bado ni changa , hiyo itasaidia katika kile kizazi kinachotoka katika familia yangu kukua katika misingi ya kuamini zaidi katika Neno la Mungu .


Familia yangu yaani watoto wangu nikiwajengea mizizi ya kumcha Mungu katika roho na kweli siku za usoni .

Neno la Mungu inatakiwa lianze kufundishwa katika ngazi ya kifamilia  na hilo ni jukumu la baba na mama , na hapo ndipo wanapojiandalia familia yenye hekima na busara au familia ya wapumbavu, katika suala hili kunahitajika umakini wa hali ya juu sana kwasababu  wale watoto mnaoanza kuwajenga  kwenye mazingira ya kumcha Mungu na ambayo ni hatua ya kwanza , hatua ya pili ni kwamba watoto inatakiwa wayashuhudie matendo mema na maneno yenye hekima na busara katika vinywa vya wazazi wao.

Mzazi akiwa ana tabia ya kunena maneno yaliyoko kinyume na mapenzi ya Mungu au kufanya matendo yasiyompendeza  Mungu. Mfano wa matendo ;Baba  kumpiga Mama watoto wakiwa wanaona au Baba kumtukana Mama watoto wakiwa wanasikia , na wakati huohuo watoto wanaona mnashiriki katika mafundisho ya Neno la Mungu  kanisani na mnaleta Wachungaji nyumbani na wazazi hamna  mabadiliko yoyote , maana yake mnaandaa kizazi cha nyoka kwenye familia yenu na ambacho kitakuwa kimefunikwa na jina la Yesu Kristo juu lakini ndani ni mbwa mwitu.

Inatakiwa nichunge sana kufanya makosa kwa namna yoyote ile mbele ya mtoto akiona , kwasababu mimi ndiye mwenye dhamana ya kuijenga familia  yenye ufahamu na familia isiyokuwa na ufahamu 1Yohana 1:1-6.

Ninaipenda sana injili ya Yesu Kristo , kwasababu Kristo ndiye ambaye ameleta Neema na kweli , yaani ndiye ambaye ameleta wokovu utakaouturithisha  Ufalme wa Mungu  ndio maana dunia haikuishia kipindi cha Musa, lakini dunia itaishia  katika kipindi cha Yesu Kristo hakuna mwingine tena Yohana 1:16-18.

Nikiisoma Biblia au nikakaa chini  nikasikiliza Neno la Mungu nikiwa bado sijaokoka hiki kitabu kitakuwa kwangu ni historia yaani  hakitakuwa na msaada na mimi , kwasababu jina la Yesu Kristo linafanya muujiza wowote ule kwa mtu ambaye amejiunganisha  na wokovu ni Yesu Kristo , ndiyo maana 1Wakorintho 6:17 imefunua jambo hili  wazi.

Nikiwa ni mkristo ninayeenda kanisani kila siku lakini bado sijamkiri na kumwamini Yesu Kristo maana yake sijaokoka kibiblia ninaitwa mtu ambaye sio roho moja na Yesu Kristo, ndio maana watu wengi wanaishia kwenye mataabiko  ,Kivipi? Wanataka uponyaji lakini hawataki kumwamini kwamba yeye ni mwokozi wa maisha yao.

Katika suala zima la kijiendeleza kiufahamu  kunahitajika haekima ya Neno la Mungu katika maisha ya mtu, kwasababu Neno la Mungu ndilo limepewa dhamana na Mungu katika kuyajenga maisha ya mkristo  na kuyaimarisha kiroho.

Nikitaka makusudi ya Mungu yathibitike kwenye maisha yangu  mimi inatakiwa  niambatane na Neno la Mungu  yaani tuwe wamoja  , na ili niweze kujitambua mimi binafsi kwamba maisha yangu  yameambatana na Neno la Mungu kuna mambo haya yatajitokeza  kwangu:-
A)Sitapenda muda mwingi upite bila kushika Biblia kusoma.

B)Nitakuwa mtu ambaye wakati wangu wa kuomba ninasimamia Maandiko yaliyoandikwa ndani ya Biblia.

C)Nitajitahidi kuwa mtu ambaye wa kuhudhuria mafundisho na kutokukubali kupitwa  na mwongozo wowote ambao kiongozi wangu  wa kiroho anautoa .

Nikisema ninamwamini Yesu Kristo na kumkiri na wakati huohuo  bado nina matendo ya giza kibiblia ninaitwa mnafiki.

Inatakiwa nijitahidi kuliishi Neno la Mungu ili nipate kibali ndani yake cha kuyaishi maisha Matakatifu, vilevile kushinda madhaifu mabalimbali.

Jambo la kufahamu Neno la Mungu lina rekodi ya maisha  ya kila mwenye mwili , ndio maana lina uwezo wa kumponya mtu, lin uwezo wa kufufua , lina uwezo wa kubariki , vilevile lina uwezo wa kumrithisha mtu ufalme wa Mungu hii yote inatokana na Neno  ndiye Mungu mwenyewe Yohana 1:1-3.

Neno ana mamlaka ya kila kitu lakini anafanya kazi  na mtu anayemwamini Yesu kristo , kwasababu Yesu mwenyewe ni sehemu ya huyo Neno Yohana 1:14.

Katika nyakati zilizopita yaani za Agano la kale  utukufu wa Neno ulionekana katika mazingira ya kimwili , ndio maana hata wakina Petro, Yohana na Yakobo walitembea na Yesu  wakapanda mitumbwi wote pamoja wakaenda Getsemane bustanini kuomba walikuwa  katika mazingira ya kimwili , baada ya hapo Yesu alivunja nguvu ya Agano la kale na kuivalisha Agano jipya  nguvu , hata maandiko yanathibitisha  katika Waebrania 7:21-22, Waebrania 8:6 na Waebrania 12:23-25.

Nikifundishwa Neno la Mungu na mtu ambaye  naye ameenda darasani kusoma neno hilo  litakuwa na mapungufu makubwa  sana Kivipi? Litakuwa halitoki katika mtiririko  wa Roho Mtakatifu, bali litakuwa linatoka katika ufahamu wa kishule,na wote tunafahamu ufahamu wa kishule  ni kuiendeleza akili , bali ufahamu wa Roho Mtakatifu ni kuiendeleza roho , kwahiyo ikiwa mimi ni mkristo niliyeokoka kweli  ninahitaji kusimama na Mungu   inatakiwa nikae chini ya Mtumishi wa Mungu  anayeongozwa na Roho Mtakatifu katika kitabu cha Warumi kimeyafunua zaidi  Warumi 8:14.

Wakristo wengi wameshindwa kuimarika katika misingi ya kiimani na roho zao zimebaki na hali ya upweke , kwasababu mafundisho wanayojengwa nayo ni ya historia  na siku zote historia haina uhai ndani yake  ya kutengeneza  wazo jipya, ndio maana maisha ya walokole wengi yamedumaa, na hii inatokana na kufundishwa historia tu.

Injili ya Yesu Kristo  inatupa mwanga na ufahamu  wa namna ambavyo tutaitimiza wokovu katika haki na kweli , ndio maana Biblia ikasema katika Waebrania 12:24.

TAHADHARI
Inatakiwa niyachunge maisha yangu  ya  wokovu nisije nikayachanganya  na watu ambao wanaopinga kazi  za Roho Mtakatifu lakini unaweza kukuta saa zingine  ni viongozi  wa kiroho au ni watu ambao waliokoka muda mrefu, kwanza  nifahamu kazi za Roho Mtakatifu:-
i)Uponyaji katikati ya kundi
ii)Ishara katikati ya kundi
iii)Miujiza katikati ya kundi
 iv)Mafunuo ya Neno la Mungu
v)Madhihirisho yote ya Roho Mtakatifu maana yako mengi sana , kwahiyo nitakapokuta mahali popote hata iwe kwenye nyumba ya ibada kazi za Roho Mtakatifu zinapingwa sehemu hiyo  inabidi niikimbie maana ina laana

Je laana  inatokana na nini?
Laana inatokana na kupinga maneno yaliyotoka katika kinywa cha Yesu Kristo Yohana 14:12,Yohana21:25, Marko 16:17, kabla hujapinga kazi  za Roho Mtakatifu hakikisha umesoma Biblia na umeielewa.

Watu wengi tunashindwa kulitumia jina la Yesu Kristo  kutuletea mabadiliko  na kutubariki , kwasababu  bado hatujawa na imani  ya kuamini kwamba tunamwamini Yesu  ingawa tunasema  tunaamini , na chanzo cha matatizo hayo yote  ni kukaririshwa historia  ya Biblia.

Watu wengi maisha yao yanalaanika , kwasababu wanatabia ya kupenda kusikiliza sana maneno  ya watu ambao wanapinga kazi za Roho Mtakatifu, kwahiyo hujikuta na wao wameshaingia katika ule mkumbo , ndio maana hata idadi ya vifo  inaongezeka kila siku  kabla ya wakati  wa umri ulioandikwa  kwenye Biblia .

Imani ni msingi wa maisha ya mkristo anayetumainia siku moja kuurithi ufalme wa Mungu , kama mimi ni mmoja wapo  kati ya wale wenye matumaini  inatakiwa nifanye mambo yafuatayo:-
A)Niwe mtu mwenye kupenda  kusikiliza Neno la Mungu  na kuhudhuria vipindi vya kanisani .

B)Niwe mtu mwenye kupenda kujisomea Biblia na kupenda kujisomea vitabu mbalimbali vya Watumishi wa Mungu waliotumika na Roho Mtakatifu.

C)Niwe mtu mwenye mbinu mbalimbali za kujiongeza kiufahamu kwasababu hali ya kujiongeza   ndiko kunakotokea tendo la ukuaji wa kiroho (kiimani)



Hakuna maoni: