Jumapili, 14 Septemba 2014

PALILIA IMANI sehemu ya pili.



14/09/2014 JUMAPILI
UJUMBE WA LEO:  PALILIA IMANI.
SEHEMU YA PILI.
KIPENGELE (B) KUPATA MAMLAKA YA NENO (UUMBAJI)

Ili niweze kutumia vizuri mamlaka niliyopewa inatakiwa nifahamu kwanza chanzo cha mamlaka yangu ni wapi au ni nini.

Chanzo cha mamlaka ya mkristo anayemwamini Yesu Kristo ni Neno  la Mungu , na hii inategemea namna ambavyo mwamini ana kina katika kuliamini Neno la Mungu.

( Kina cha imani ndicho kinazaa mamlaka yenye nguvu ya kuumba jambo likatokea).

Waamini walio wengi hawalisomi Neno la Mungu (kulisikiliza) katika misingi ya imani ndio maana mamlaka ndani mwao hukosa nguvu ya kubomoa aina za vipingamizi wanavyokabiliana navyo katika maisha yao ya ukristo.

( Kama mwamini haliamini Neno la Mungu katika kina maana yake mamlaka alioyo nayo imekufa).

Mimi kama mkristo mwamini inatakiwa nifahamu Neno la Mungu ninalolisoma ni hai,kwahiyo nikilisoma Neno hilo lazima nilisome katika misingi ya kiimani,hata Biblia imeyathibitisha haya katika Waebrania 4:12.

Mkristo anayeishi maisha ya ukweli ,yaani yaliyo sambamba na maandiko matakatifu yanavyosema huyo ndiye mkristo mwenye mamlaka iliyo hai.

Maandiko matakatifu yanakuwa hai kwa mkristo mwamini anayeishi maisha ya ukweli na huyo ndiye mkusudiwa katika ufalme wa Mungu.
Ø  Mkristo asiye tii ndani ya kanisa anachoelekezwa na Mtumishi wa Mungu maana yake huyo ni mtalii wa kiroho.
Ø  Mtalii wa kiroho huwa ana sifa hizi:-
i)Huwa ana imani ya tomaso.maana ya imani ya tomaso huwa haamini anachoambiwa mpaka kitokee ndipo aamini
ii) Huwa hakubaliani na mwongozo anaopewa na Mtumishi wa Mungu na kumfanya atoke katika shida aliyonayo,bali yeye hupenda kuwekewa mikono , ndio maana utamkuta anatangatanga katika makanisa tofautitofauti.
iii) Huwa ni mtu anayeihangaisha roho yake na kuinyima uhuru wa kumtafuta Mungu,kwahiyo mtu wa aina hii amefarakana na Baraka za Mungu.

Biblia inathibitisha katika Waebrania 4:12  kwamba Neno la Mungu li hai lakini litakuwa hai kwa mkristo mwenye imani ya Neno la Mungu(Yesu Kristo).

Nguvu ya Neno la Mungu  ndio mamlaka yenye uwezo wa kuamuru chochote kikathibitika, kwahiyo nikitaka hii mamlaka iumbike ndani mwangu inatakiwa nifanye mambo makuu mawili yafuatayo:-
i)Kulisikiliza Neno la Mungu mara kwa mara hii ipo katika misingi ya ufundishwaji.
ii) Kulisoma Neno la Mungu mara kwa mara, hii ipo katika misingi ya kuielimisha roho yangu kuhusu Neno la Mungu katika kina zaidi.

Mahali ombapo moyo na roho hukutana ni kwenye faragha, na katika faragha hiyo ndipo Mungu hupitishia taarifa zake.

Faragha ni sehemu ya utulivu na usikivu ndani ya moyo wa mkristo anayemwamini Yesu Kristo.
Ili niweze kufahamu neno hili ninalolisoma li hai ndani mwangu ni pale litakapoyagusa mapenzi  yangu.

( Siku zote mapenzi ya mwanadamu hayana utukufu kwa Mungu,ndio maana mamlaka za wakristo zimekuwa butu).

MFANO;Panga lina sifa ya kukata likiwa butu haliwezi kukata maana yake sifa ya panga imepotea;Ndivyo ilivyo kwa mkristo mamlaka aliyonayo inanolewa kwa Neno la Mungu,asipo noa mamlaka yake kupitia Neno la Mungu atakapokutana na majaribu hataweza kupenya.

ANGALIZO :Inatakiwa nijihadhari sana vilevile niwe na bidii sana katika kuliamini Neno la Mungu, kwasababu ninaweza kujikuta ninaitwa mkristo katika mwili lakini katika roho ni mpinga kristo namba moja,hii inatokana na namna ambavyo ninakataa kuingiza maarifa ya Mungu ndani mwangu yaniongoze.

KINACHO ATHIRI MAMLAKA YA MTU.

Kila mkristo anayemwamini Yesu Kristo yaani aliyeokoka tayari anayo mamlaka.

Yapo mambo mengi yanayoweza kuathiri mamlaka ya mkristo,lakini kuna jambo moja kuu ambalo ndilo hupoteza kabisa uwezo wa mamlaka ya mtu kufanya kazi

a)Maneno yasiyokuwa na maana.
Maneno yasiyokuwa na maana katika kinywa cha mkristo mwamini ni sumu inayozima nguvu ya imani ipoteze uwezo wa mamlaka

Inatakiwa niwe makini katika kauli zangu,kwasababu kauli zangu ndizo zinazothibitisha mahusiano yangu na Mungu kwa jamii inayonizunguka.

( Maneno yangu mimi ndio yanayofunua siri ya moyo wangu kwa watu wengine)

Maneno ya kinywa changu ndio yanayothibitisha moyo wangu umejawa na kitu gani.

Nikijifahamu mimi kwamba ninamkiri Yesu Kristo na kumwamini yaani ninaishi katika maisha ya wokovu inatakiwa niwe na tahadhari katika kunena kwangu,kwasababu Biblia imetahadharisha kitu yaani ukamilifu wa mkristo unatokana na Yakobo 3:2b.

Ukamilifu wa mkristo anayemwamini Yesu Kristo upo katika Neno.

Mkristo mwamini akilinda kinywa chake atakuwa ameiokoa mamlaka aliyonayo hapo ndio utakuwa mwanzo wa mamlaka hiyo kumsababishia Baraka.

Mkristo mwenye mamlaka kazi yake ni moja kuamuru vimrejee alivyoibiwa na shetani.

Ili niweze kuipalilia mamlaka niliyo nayo inatakiwa nilazimishe kinywa changu kunena kweli hata kama mazingira hayaruhusu kwa muda huo , kusema ukweli,lakini nitakaponena kweli katika kinywa changu Roho Mtakatifu ataingilia kati kuleta msaada kwangu.

Kuongezea maneno yasiyo ya kweli katika kauli zangu za kweli kuna athiri mahusiano yangu na Roho Mtakatifu, huo ndio mwanzo wa Roho Mtakatifu  kumkimbia mtu, kwasababu Roho Mtakatifu ni kweli ataishi kwa mtu anayeishi maisha ya ukweli.

Nikiishi sambamba na ndio yangu ni ndio na sio yangu ni sio nitaambatana sambamba na Baraka za Mungu.



Hakuna maoni: