Jumapili, 7 Septemba 2014

AMINI UNALO KUSUDIA LITATIMIA TU



                                            5/09/2014
AMINI UNALO KUSUDIA LITATIMIA TU.
 
Maisha ya kiimani ninayafananisha na mkulima ndani ya shamba,kwasababu mkulima huwa ana tabia ya uvumilivu akingojea nyakati za mvua na majira yake ili aweze kuvuna,yaani jambo hili kwa mkulima hulifanya katika mazingira ya kiimani zaidi.


Kinacho umiza imani za wakristo walio wengi huwa wanashindwa kutambua nyakati za kubarikiwa na nyakati za kuimarishwa kiimani (kujaribiwa).

( Kujaribiwa ni nyakati za mwamini kuimarishwa kiroho ,nyakati hizi jamii ya waamini walio wengi huwa hawaipendi,lakini hushindwa kutambua imani huongezeka kulingana na jinsi unavyokutana na misukosuko(majaribu).

Inatakiwa niwe makini sana na neno hili ni tahadhari kwangu yaani wakati wa kupitia katika majaribu mbalimbali inatakiwa jambo ninalolikusudia moyoni mwangu kwamba Mungu atalitimiza niliamini tu bila kuvunjika moyo mwisho wa siku litatimia machoni pangu hata kama litachelewa.

Ninachotakiwa kufanya kama mkristo mwamini jambo ninalolikusudia moyoni mwangu na kulitamani kwamba Mungu atanitendea inatakiwa niamini jambo hilo ndipo mipenyo itakavyofunguka ,kwasababu Mungu anatazama kiwango cha imani aliyonayo mtu juu ya jambo lile analolikusudia moyoni mwake.

Nikiamini juu ya jambo ninalolikusudia moyoni mwangu , maana yake ninakuwa nimeandaa mazingira ya wepesi wa jambo hilo kutimia bila kutazama mazingira gani niliyonayo ,ndio maana Biblia ikasema Ayubu 22:28.

Nikiyaamini maombi yangu ninayoyaomba kwenye uso wa Mungu,Roho Mtakatifu ataweka wepesi wa maombi hayo kujibiwa haraka,kwasababu nitakuwa nimeomba katika misingi ya kiimani zaidi.

Kitendo cha mimi kukusudia jambo ninaloliamini moyoni mwangu kwamba Mungu atalitenda itanisaidia kunipa muunganiko wa Roho Mtakatifu, hapo naweza kuitwa mkristo ninaye muomba Mungu katika misingi ya rohoni.

Kunia jambo ndani ya moyo ndiko kunakotengeneza mpenyo katika maisha ya mtu ,kwasababu kitendo cha mimi kunia jambo maana yake ninaliamini jambo hilo katika kina zaidi.

( Thamani ya nuru ni wakati giza likiwepo).

Thamani ya imani ya mkristo huonekana pale ambapo inamtatulia majaribu yaliyo mzunguka .

Ili imani yangu ionekane ni ya thamani machoni pa Mungu inatakiwa nisimame katika jambo lile ninalolikusudia moyoni mwangu mpaka litakapo timia, na jambo hili lahitaji mtu binafsi kujitoa
.
Mkristo ambaye bado anaishi katika ulimwengu huu hawezi kuyaepuka majaribu,bali ni kumuomba Mungu aweke wepesi wa kuyavuka majaribu bila kuathirika kiimani.

Nikiwa ninaishi katika mwili siwezi kuyakwepa kujaribiwa, ndio maana Mungu alinena na Yoshua na kutoa maagizo kwake ili asivunjike moyo Yoshua 1:1-18.

Yoshua 1:5 inathibitisha namna ambavyo Mungu alijiaminisha kwa moyo wake wote kuhusu utumishi wa Yoshua,ndivyo ilivyo hata leo nikisimama vizuri katika misingi ya kiimani maneno haya yatakuwa hai kwangu.

Nikitaka kugundua imani yangu ni kipofu nitazame maisha ninayoishi, ninaweza kuwa nimeokoka sawa lakini matendo yangu yakapingana na wokovu nilionao
“ Ee Yesu nisaidie matendo yangu yaendane na utumishi wangu”.

Haijalishi ni mazingira gani ninayoyapitia katika maisha yangu ya wokovu bali imani yangu inatakiwa ing’ang’anie katika lile ninalolikusudia moyoni mwangu kwamba Mungu atalithibitisha.

AMEN.

Hakuna maoni: