Jumapili, 24 Agosti 2014

ANGUKO LA WAKRISTO SEHEMU YA PILI



24-08-2014
ANGUKO LA WAKRISTO SEHEMU YA PILI
UTII
Maisha ya wakristo waamini yameathirika kiuchumi, kifamilia, kielimu,kiafya, hii inatokana na kuto kutii muongozo wanaopewa na watumishi wa Mungu katika kukabiliana na matatizo yao.

Inafahamika wazi utii una asili ya unyenyekevu ,kwahiyo mkristo akiwa ni mtii katika miongozo anayopewa na kiongozi wake wa kiroho, changamoto yoyote itakayo jitokeza katika maisha yake ya ucha Mungu, atakuwa na nafasi kubwa ya kushinda.

Ushindi wa maisha ya mkristo umejificha ndani ya utii, hili jambo waamini wengi hawajaligundua kwamba Baraka zao zimejificha wapi.

Mfano katika hali ya kibinadamu: Mwanadamu anapo umwa (kuugua) hawezi kufika hospitali daktari akampa dawa tu! Lazima atamuingiza kwanza kwenye vipimo , ili atafute kufahamu ni ugonjwa gani unamsumbua ili aweze kupewa dawa sambamba na ugonjwa alio nao; sasa basi katka hali ya kiroho mkristo anapokwenda kwenye uso wa mtumishi wa Mungu akihitaji msaada wa kuponywa shida aliyonayo,inatakiwa muongozo atakaopewa na Mtumishi wa Mungu kulingana na shida aliyonayo kwa hapo haijalishi ni mwongozo wa aina gani,labda anaweza kuambiwa hudhuria kanisani utafunguliwa,au chukua maji unywe yaliyoombewa,au soma Biblia kifungu Fulani,huu mwongozo kitendo cha mwamini kuutii lazima afunguliwe,lakini asipoutii mwongozo huo atazidi kuathirika mara dufu,kwasababu Mtumishi wa Mungu mwongozo anaoutoa unatoka  kwa njia ya Roho Mtakatifu,kwa maana zaidi anakuwa amekaidi waziwazi sauti ya Mungu mwenyewe kupitia Mtumishi wake,Biblia imefunua wazi juu ya utii,vilevile imeainisha Baraka zitakazo ambatana na mwamini anayeiheshimu sauti ya Mungu Kumbukumbu la Torati 28:1.

( Utii humsogeza mwamini karibu  sana na Baraka za Mungu).

Mkristo anapokuwa mtii katika agizo analolitoa Mungu kupitia Mtumishi wake katika roho,mkristo huyo hupata kibali ambacho ndicho husaidia mwamini katika hali ya kimwili kutokupungukiwa kamwe na Baraka za Mungu.

Utii hufungua milango ya ufahamu wa rohoni katika maisha ya mwamini,ndio maana Mungu kaweka wazi kupitia Kumbukumbu la Torati 28:2 baraka atakazo ambatana nazo mwamini akiwa na asili ya utii; jambo hili lahitaji ufahamu zaidi kwasababu kila kitu kimefunuliwa wazi kuanzia mstari wa pili na kuendelea.

Chanzo cha mkristo mwamini kupiga hatua katika maisha yake ya wokovu ni pale atakaporuhusu hali ya utii wa maagizo anayoyatoa Mungu kupitia watumishi wake.
Anguko linalowakumba wakristo na kusababisha maumuvu yasiyoponyeka ni pale ambapo wakristo hao kukaidi sauti ya Roho Mtakatifu.

ANGALIZO 1:Ninapoikaidi sauti ya Roho Mtakatifu maana yake ninamkufuru Roho Mtakatifu nikiwa nina akili zangu timamu,ndiyo maana unaweza ukamkuta mtu yuko juu sana kimaisha, ghafla akapukutika akawa hana kitu ni kwasababu ya kukaidi agizo moja tu ambalo Mungu analitoa kupitia watumishi wake,watu wa aina hii Mungu amefunua wazi mapigo watakayoambatana nayo katika maisha yao inaonesha kuanzia Kumbukumbu la Torati 28:15….

Maisha ya wakristo waamini yameathiriwa na laana ambazo hutokana na kukaidi agizo la Roho Mtakatifu.

ANGALIZO 2:Siku zote hakuna madhabahu inayomtangaza Yesu Kristo wa Nazareti na udhihirisho wa Roho Mtakatifu ukaonekana mahali pale watu wakiponywa, wakifunguliwa, wakirejeshewa afya njema halafu madhabahu hiyo ikasababisha umasikini kwa watu au matatizo kamwe haipo wala haitatokea milele, bali wakristo wengi ni wavivu kutendea kazi miongozo wanaypopewa na watumishi wa Mungu,kwasababu huathiriwa na hali ya kulizoelea kanisa.

( Nikiruhusu haki ya Mungu kuniongoza (mapenzi ya Mungu) mimi nitakuwa ni mtu wa tofauti katika jamii).

Hakuna dhambi mbaya kama ya kukaidi agizo la Roho Mtakatifu analolitoa kwangu na wakati huohuo liko ndani ya uwezo wangu kulitendea kazi kama nikiamua.

Maisha ya walokole yamekosa mipenyo ya Baraka za Mungu, kwamaaana zaidi yamefarakana na Baraka za Mungu kwasababu ya majivuno ya mambo yafuatayo:-
a.     Hata mimi ninajua kuomba
b.     Hata mimi ninaweza kufunga nikamlilia Mungu akanisikia, kwani! Siunajua Mungu hujifunua kwa yoyote hana upendeleo.
c.      Hata mimi ninaweza kunena kwa lugha , haya ndiyo mambo yanayo wadidimiza walokole wa leo wadidimie kimaisha, vilevile na umaskini usiondoke katika nyumba zao, walokole hujisahau na kitu hiki hawakitambui, mpakwa mafuta yaani mtumishi aliyeitwa kwa jina la Bwana ambaye elimu hiyo anayo ihubiri hakuipata kwa mtu yeyote wala mahali popote  isipokuwa kutoka kwa Mungu kwa uwezo wa Roho mtakatifu, huyo mtumishi ni jicho la Mungu, utakapo tii agizo atakalo kupa maisha yatabadilika jumla wala hautaishi maisha ya kushindwa kwasababu agizo la Mungu huja kwa njia ya Roho mtakatifu kumfahamisha mtumishi wake, na mtumishi wake kutoa muongozo kwa kanisa , ndio maana Biblia inamheshimu sana mwamini aliye chini ya muongozo wa Roho mtakatifu.
Warumi 8:12-16

ANGALIZO 3: Nikitaka kufanikiwa katika maisha ya wokovu niache tabia ya kulizoelea kanisa , kwasababu kulizoelea kanisa  husababisha madhara kwa watu wengi wa Mungu, na madhara hayo hutokana na kupuuzia agizo linalotoka kwa mtumishi wa Mungu, hichi kitu ndicho kinacho didimiza kanisa mazoea.

( Atakaye chota Baraka za Mungu ni yule anayeendana sambamba na maagizo ya Mungu).

Kinacho wafanya wakristo washindwe kuinuka kimaisha ni hali ya mazoea wanayoiruhusu katika maisha yao na inafahamika wazi tabia ya mtu ni jumla ya mazoea yake.

( Kama ninahitaji mabadiliko katika maisha yangu ya wokovu ninatakiwa nipingane na hali ya mazoea, bali niruhusu utii wa kila agizo nitakalo lisikia mtumishi wa Mungu akiliagiza, hapo nitafanana na Baraka za Mungu).

Hakuna maoni: