Jumapili, 2 Novemba 2014

VITA VYA KIIMANI SEHEMU YA PILI.



2/11/2014
VITA VYA KIIMANI: SEHEMU YA PILI.
Vita vya kiimani  vinapiganwa  katika mazingira ya rohoni, ndio maana vinaihusisha imani kwa asilimia mia moja , na hii yote inatokana na imani ,kwamba ni kitu cha rohoni na siku zote kitu ambacho kipo rohoni hakina umbo maalumu.


Imani  haishikiki kwa mkono wala haina umbo maalumu vilevile ni kitu kilichokamilika, ndio maana sisi tunaomwamini Yesu Kristo tunasisitizwa sana kudumu katika misingi  ya imani , na hapo ndipo unapotokea mpenyo wa maisha ya mtu kueleweka  vilevile kufanikiwa.

Wakristo wengi  wamejichanganya vita vya kiimani wamevigeuza ni vya kimwili ndio maana maisha yao yameishia kubeba hila na kujeruhika.

Vita vya kiimani  vinapiganwa kiroho na sio kimwili.

Nikivigeuza vita vya kiimani  (kiroho) katika hali ya kimwili lazima nitashindwa kwasababu anayeni[pigania anaishi katika Roho.

Vita vya kiimani havipiganwi kati ya mtu na mtu bali vinapiganwa kati ya mtu na madhaifu yaliyoko kwake.

MFANO: Mimi nina tabia ya uongo tayari ile tabia ndio shetani  katika maisha yangu, vilevile kipingamizi kitakachomzuia Mungu asiseme na mimi.
 
Vita vya kiimani ni kati yangu na dhambi inayokula maisha yangu.

(Hii ni hatari sana wakristo wengi wataikosa mbingu kwasababu ya kukubali kuaminishwa kinyume na Maandiko Mtakatifu).

Ni vigumu kuingia kwenye uwanja wa mapambano ukiwa  hauna uzoefu wa kutosha wa kutumia silaha adui atakumaliza, hii ni sawa na mkristo anayeingia katika vita vya kiimani  yaani katika uwanja wa mapambano  akiwa bado hajatubu dhambi.

Vita vya kiimani vinamhitaji mkristo mwenye   upeo wa ufahamu wa Rohoni wa kutosha.

Mahusiano na Neno la Mungu (Biblia) na mkristo ndiyo yatakayomsaidia kupenya kwenye ulimwengu wa roho,kwasababu vita vya kuyaharibu maisha ya mkristo havianzii katika mwili vinaanzia katika  Roho.

Mwenye uwezo wa kuvishinda vita vya kiimani  ni mkristo aliyeimarika katika Neno la Mungu.

Silaha itakayomsaidia mkristo kushinda vita vya kiimani  ni Neno la Mungu (Biblia) na jambo hili limethibitishwa wazi katika  Waefeso 6:10-23.

Ili mkristo aweze kuvishinda vita vya kiimani inatakiwa aungane na Neno la Mungu kwa maana zaidi yeye na Neno ni wamoja,huyo anaweza kuitwa mkristo aliyekamilika kiroho.

Jinsi ninavyopoteza uwezo wa kusoma Biblia ndivyo ninavyomwongezea shetani  nguvu na uwezo wa kuyavamia maisha yangu.

Nikiona nguvu ya kusoma Biblia kwangu imeondoka nijue kabisa ipo nguvu  ya kipepo imenivamia na nisipokuwa makini itanidhalilisha.

Wakuu wa ulimwengu huu wa giza ambao ndio napambana nao katika vita vya  kiimani hawaji kwangu katika umbo la kibinadamu bali wanakuja kwangu katika umbo la madhaifu mbalimbali,kwahiyo  nisipokuwa na upeo wa kutambua  nitajikuta tayari nimeshakuwa mtu wa kudhalilika .

Na mazingira wanayoyatumia wakuu wa giza kuharibu maisha ya wakristo ni kama haya:-
i)Kuujaza moyo wangu hasira muda wote,hii yote ni ili nisiwe mtu wa kusamehe.
ii)Kunijaza hila kwenye moyo
iii)Kunivalisha tamaa ya mwili na mali.
iv)  Kunisukuma zaidi katika hali ya kusema zaidi uongo,haya pamoja na mengine mengi ndiyo yanayotumiwa sanasana na akuu wa giza wa ulimwengu huu lengo ni kuharibu mfumo  wa mtu anayemcha Mungu.

Hakuna maoni: